Kiungo Mshambuliaji kutoka Zambia Clatous Chama amewaaga rasmi Wanasimba, baada ya kukamilisha taratibu za kujiunga na RS Berkane ya Morocco.
Chama ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kutoa neno la kwaheri na shukurani kwa waajiri wake hao wa zamani.
Chama ameandika: “Nimekuwa kimya kwa muda tangu mara ya mwisho nitume ujumbe wowote kwenye kurasa zangu za kijamii, ilibidi iwe hivyo kwa sababu kuna mambo nilikuwa ninakamilisha na nilikuwa nasubiri taratibu zote zikamilike, siwezi kuwaacha nyinyi kwenye giza,”
“Stori yangu ilianza pale nilipokuja Tanzania Mwaka 2018, sikuwa najua kwamba ningeweza kuwapata watu wengi kuweza kuongea Kiswahili lakini upendo ambao nimeweza kuupata hapa hauelezeki katika maisha yangu,”
“Siwezi kueleza namna ninavyohisi kuhusu Simba, kwa maneno machache ni kwamba bado ni ngumu kuamini kwamba jina langu halitatajwa na Baraka Mpenja msimu ujao ama sitavaa jezi yangu namba 17, katika timu ambayo ilikuwa ni ya nyumbani,”
“Asante kwa viongozi wa Simba, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mr Mo Dewji, CEO, Barbara Gonzalez, uongozi wa timu kiujumla, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenzagu pendwa asanteni kwa upendo wenu,”
“Kwa mashabiki nitazidi kuwakumbuka nasema asante sana nitazidi kuwasiliana nanyi kupitia mitandao ya kijamii, nitaendelea kushangilia pamoja nanyi labda ikitokea nikacheza nanyi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa heri na asanteni,”
ASANTENI SANA