Kikosi cha Azam FC leo Jumatatu (Agosti 23) kimeelekea nchini Zambia kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na Msimu mpya wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.
Azam FC waliondoka mapema Alfajiri kuelekea mjini Ndola ambapo watakuwa huko hadi mwanzoni mwa mwezi Septemba.
Kocha Mkuu wa matajiri hao wa Chamazi George Lwandamina anatajwa kuwa kichocheo kikubwa kwa kikosi chake kuweka kambi mjini Ndola, Zambia.
Tayari Uongozi wa klabu hiyo umeshatangaza ratiba ya michezo ya kimataifa ya kirafiki kwa kikosi chao kitakapokua kambini.
Azam FC itacheza michezo minne ya Kimataifa ya Kirafiki dhidi ya Red Arrows FC (25/08/2021), Zanaco (29/08/2021), Forest DC (02/09/2021)
na Zesco FC (03/09/2021).
Azam FC itashiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Africa ‘CAF’ itakayoanza rasmi Septemba 15.
Wakati huo huo Afisa habari wa klabu ya Azam FC Thabit Zakaria (Zakazakazi) amesema wamesitisha tamasha la Azam festival ambalo ilikuwa lifanyike hivi karibuni kwasababu ratiba imewabana sana.