Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umekanusha taarifa za kufanyika kwa Tamasha la Simba Day siku ya Jumamosi (Agosti 28).
Kaimu Afisa Habari wa Simba SC Ezekiel Kamwaga amesema taarifa za kufanyika kwa Tamasha la Simba Day kwa tarehe inayotajwa hazina ukweli wowote huku akiwataka mashabiki kuwa na subra.
Amesema Uongozi wa Simba haujawahi kutangaza popote tarehe maalum ya kufanyika kwa Tamasha hilo, ambalo kila mwaka huwakutanisha kwa pamoja Mashabiki na Wanachama Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es aalaam.
“Taarifa mlizokuwa mkiziona Kuwa Simba Day itakuwa ni Tarehe 28 hazikuwa rasmi klabu ya Simba Haijawahi kutangaza popote kuwa Simba Day itakuwa ni lini, Ila niwatoe hofu Mashabiki wa Simba kuwa mwalimu aliomba kupewa muda zaidi ili akisuke Kikosi chetu Cha Simba”
“Bado kikosi chetu kitakuwepo nchini Morocco mpaka mwisho wa mwezi huu ili kujifua zaidi,”
“Mwenyekiti wa klabu yetu nadhani wiki hii atawatangazia kuhusu Tarehe ambayo tamasha letu la Simba Day Iitafanyika na tamasha hilo litafanyika mwezi ujao (Septemba).” amesema Kamwaga.
Simba SC hutumia Tamasha la Simba Day kuwatambulisha wachezaji waliosajiliwa kwa msimu mpya, sambamba na kucheza mchezo wa kimataifa wa kirafiki.