Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amesema tukio la mauaji ya askari wanne lililotokea juzi jijini dar es Salaam ni tukio kubwa kwa Jeshi la Polisi lakini ndio kazi ya askari, na sasa wamepata kitu cha kujifunza kama askari, wananchi wao wana kitu cha kujifunza na wafiwa nao wana kitu cha kujifunza.

Amesema hayo wakati wa kuaga miili ya Askari hao leo Augost 27, 2021 katika viwanja vya Polisi, Kurasini Jijini Dar es Salaam.

“Ukishakuwa na mtoto mhalifu, mwizi, gaidi au mwenye tabia mbaya mbaya usiposhirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuna mawili anaweza akaleta madhara kwa Watanzania ama uhai wake ukapotea” Amesema IGP Sirro

“Huyu Hamza aliyoyafanya kama ndugu zake wangewajibika vizuri leo tusingekuwa hapa, lakini Watanzania wajue kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo kwa ajili ya kulinda usalama wa Watanzania, ndio maana tumeapa kwa Amri Jeshi Mkuu kufa kwa risasi, hatuoni tabu”.

“Lazima Watanzania wajue kwamba na sisi tuna familia zetu, ukishajua kwenye familia yako kuna mhalifu ujue wewe ni tatizo kwa Watanzania, tunategemea uzae mtoto ambaye kesho atakuwa Waziri, IGP au mwalimu, lakini ukizaa mtoto akawa mwizi, paruanja ni tatizo.

“Kwa wafiwa kuna kitu cha kujifunza, askari wetu hawakuwa magaidi, hawakuwa wezi, hawakuwa majambazi, wamekufa wakilinda Watanzania, kifo chao ni kwa heshima ya Watanzania, tusipate huzuni sana, tuwaombee kwa sababu walichokuwa wanafanya ni ajili ya kuwatetea Watanzania.

“Kwa police officers na viongozi wa ulinzi na usalama kutokana na wenzetu kufa kwa kupigwa risasi vichwani, huwa nawaambia siku zote usicheze na mtu wa hovyo hovyo, usimwamini kila mtu, hii ni kwa sababu ya imani.

“Tumepoteza vijana wadogo sana, sisi tunaokaribia kustaafu tunajua hawa ndio wangekuja kuliendesha jeshi hapo baadae, lakini kwa sababu ni sehemu ya maisha yetu. Mliobaki mmejifunza, sio kila mtu anapenda askari polisi au vyombo vya dola.

“Tuwaombee sana, wametangulia mbele ya haki na sisi tupo nyuma yao, mliofiwa si kwamba mmefiwa nyie tu, na sisi tumefiwa kwa sababu walikuwa vijana wetu, sisi tunaovaa buti bila kujali mgambo au nani huwa nasema sote ni kitu kimoja, tunalinza amani.

“Niwahakikishie ndugu wa marehemu kwamba, tutajihadi kwa mujibu wa kanuni zetu, vijana wetu hawa wanapata haki zao kama wana familia zao, watapata haki zao, niwashukuru sana, asanteni, asanteni sana,” amesema IGP Sirro.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Augusti 28, 2021
Wizara ya Afya yapokea vifaa vya milioni 300