Aliyekua Mlinda Lango wa Mwadui FC Mussa Mbisa amejiunga na Coastal Union ya jijini Tanga, tayari kwa mapambano wa Msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao umepangwa kuanza rasmi Septemba 29.
Mbisa amejiunga na ‘Wagosi wa Kaya’ kwa mkataba wa miaka miwili na tayari ameshatambulishwa na Uongozi wa klabu hiyo kupitia kurasa za mitandao ya kijamii za Coastal Union.
Mlinda lango huyo ambaye msimu uliopita alilalamikiwa na wadau wengi wa soka nchini kwa kufungwa mabao ya kizembe akiwana Mwadui FC, anatarajiwa kuwa na mwanzo mpya kwenye kikosi cha Coastal Union, ambacho msimu uliopita kilinusurika kushuka daraja.
Wakati huo huo Uongozi wa Coastal Union umetangaza majina ya wachezaji walioachwa kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Michuano ya Kombe la Shirikisho.
Orodha ya wachezaji 12 walioachwa imechapishwa kwenye ukurasa wa Instagram wa Coastal Union.