Aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Young Africans Mwinyi Zahera amewataka Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kumpa muda Mshambuliaji mpya Fiston Mayele.
Zahera amewasilisha ombi hilo, kufuatia Mshambuliaji huyo kuonesha kiwango cha kawaida alipopata nafasi ya kucheza dhidi ya Zanaco FC siku ya Jumapili (Agosti 29), akichukua nafasi ya Heritier Makambo.
Kocha huyo kutoka DR Congo amesema: Kwa Mayele ni suala la muda tu..
“Naijua Yanga, nawajua vyema mashabiki wa timu hii pia namjua Mayele. Katika mchezo dhidi ya Zanaco FC hakufanya kitu kikubwa kutokana na muda, lakini subirini acheze kisha mtakuja kunieleza ninayowaambia. Mayele ni mshambuliaji kweli kweli.”
Katika hatua nyingine Zahera amezungumzia kikosi kizima cha Young Africans kwa kusema kina wachezaji wazuri hivyo kilichobaki ni kazi kwa kocha Nabi.
“Timu ina Makambo, Mayele, Moloko na washambuliaji wengine ambao ni hatari, pia ina viungo na mabeki wazuri, hapa kazi ni kwa kocha kuijenga timu yenye kueleweka kwani kwa mchezaji mmoja kila mtu ana uwezo mkubwa,” alisema Zahera.