Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda ametoa wito kwa Vyama vya Ushirika kuangalia namna bora ya kuendeleza viwanda vinavyochakata bidhaa zinazozalishwa na Vyama vya Ushirika kwa kuongeza thamani ya mazao mbalimbali yanayotokana na vyama hivyo ili kuweza kuendana na kasi ya soko la ushindani la ndani na nje ya nchi.
Ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Pili la Kimataifa la Ushirika katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) mkoani Kilimanjaro litakalofanyika hadi Septemba 03, 2021 na kuandaliwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) huku kauli mbiu ikiwa masuala ya Ushirika na Maendeleo ya Viwanda kwa kuzingatia maslahi ya wanachama.
Waziri Mkenda amesema kuwa ni dhamira ya Serikali kuona Vyama vya Ushirika vinaongeza tija kwa kuongeza viwango vya uzalishaji ili iwe ni msukumo wa kuanzisha na kuendeleza Uchumi wa Viwanda kwa kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazotokana na Vyama, ingawa bado Sekta ya Ushirika inakabiliwa na changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege katika Kongamano hilo amesema Tume kwa mujibu wa Sheria Na.6 ya mwaka 2013 itaendelea kutekeleza wajibu wa kuvisimamia na kuhamasisha Vyama vya Ushirika, ambapo Sekta ya Ushirika ina viwanda mbalimbali 452 ambavyo vinafanya shughuli mbalimbali za uchakataji.