Umoja wa mataifa ya Ulaya (UE) umekubaliana kuunda kikosi maalumu kwaajili ya kukabiliana na mizozo mbalimbali, hili limejiri baada ya Taliban kuchukua udhibiti wa Afghanistan.
Hayo yamesemwa kwenye kikao cha EU kilichofanyika nchini Sloveni.
Washiriki wa kikao hicho wamejadili kuhusu walichojifunza kutokana na mzozo wa kuondoka Afghanistan baada ya Taliban kukamata nchi. Ujerumani imependekeza wanachama wa EU wabuni kikosi maalumu cha wanajeshi 5000, kitakachoweza kukabiliana na dharura bila kuitegemea Marekani.
Suala hilo limekuwa kwenye ajenda ya EU kwa zaidi ya muongo mmoja, lakini yaliyoshuhudiwa Afghanistan hivi karibuni yamepelekea mataifa yote 27 wanachama kulijadili kwa haraka. Mkuu wa sera za mambo ya nje wa EU Joseph Borrell amesema kwamba anatumai kwamba mpango huo utakamilika ifikapo mwezi Novemba, Pia ni Dhahiri kwamba sasa kikosi hicho kinahitajika kwa haraka.
Kuchukuliwa kwa Afghanistan na Taliban pamoja na dharura ya kuokoa maelfu ya watu kwa njia ya ndege baada ya Marekani kuamua kuondoa vikosi vyake nchini humo , kumeonesha utegemezi mkubwa wa EU kwa Marekani.
Ingawa vikosi vya EU vilikuwa vikisaidiana na Marekani wakati wa kuokoa watu, Marekani kwa sehemu kubwa ilisaidia mataifa ya EU kuhamisha watu wake.