Wahitimu wa mafunzo ya muda mfupi ya ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya milipuko wametakiwa kuacha tabia ya kukaa na ujuzi walioupata badala yake wanatakiwa kuwafundisha wenzao ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema hayo leo aliposhiriki katika Mahafali ya 14 ya mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili jijini Dae Es Salaam.
Gwajima ameongeza kuwa kwa kufanya hivyo itaboresha zaidi utendaji wa afua mbalimbali za ufuatiliaji, utambuzi wa haraka na udhibiti wa magonjwa yote ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.
Mafunzo hayo ya awali yanakusudia kutoa wataalam wa epidemiolojia katika afya ya binadamu na Wanyama ilikuongeza ufanisi wa kufanya ufuatiliaji wa afya katika ngazi ya jamii na kuweza kutambua magonjwa ya milipuko na kudhibitiwa kabla hayasababisha athari.
Mafunzo hayo yamekua yakitolewa kwa ufadhili wa Shirika la kuzuia na kupunguza matishio ya magonjwa nchini Marekani la DTRA na watumishi 41 wamehitimu kutoka Halmashauri 19 za Mikoa ya Njombe, Ruvuma na Iringa na kufanya jumla ya watumishi 512 kuhitimu kutoka mikoa 26 kwa kipindi cha miaka 6.