Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwa kushirikiana na Baraza la Michezo la Majeshi Tanzania (BAMMATA) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) wamefanya kikao leo Septemba 10, 2021 jijini Dar es Salaam kujadili mikakati ya pamoja ya jinsi ya kuendeleza michezo nchini kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkuu wa Majeshi mjini Dodoma hivi karibuni.
Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye pia ni Mwenyekiti wa BAMMATA, Brigedia Jenerali Suleiman Bakari Gwaja amesema kikao hicho kimekuwa na mafanikio makubwa ambapo kimeunda kamati ya wataalam saba na kimeipa wiki moja kuandaa mpango wa utekelezaji wa masuala yote yaliyojadiliwa ambapo yatawasiliwa kwenye ngazi ya taifa kwa ajili ya maamuzi zaidi.
“Nashukuru tumefikia azimio zuri la kuunda kamati ndogo yenye ushiriki wa pande zote tatu na tumeitaka kufanya kazi mara moja ili tupeleke mbele na utekelezaji wa mipango hii madhubuti ianze mara moja”. Amefafanua Afande Gwaja
Mwenyekiti Mwenza wa Kikao hicho, Yusufu Singo Omary ambaye pia ni Mkurugenzi wa Michezo nchini amemshukuru Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mkuu wa Majeshi kwa kutoa maelekezo ya kufanya kikao cha pamoja na kuja na mikakati ya pamoja kwa pande zote ambapo amesema itasaidia taifa kupiga hatua kwenye michezo kama ilivyokuwa kwenye siku za nyuma.
“Historia ya Tanzania inatuonyesha kuwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama ndivyo vilivilivyokuwa vikipepereusha vema bendera ya nchi yetu kwenye mashindano ya kimataifa”. Amefafanua Omary
Aidha, amesema mikakati ya pamoja iliyondaliwa kwenye kikao hiki itasaidia taifa kwenye mashindano makubwa ya kimataifa ya Jumuiya ya Madola, All African Games na Olympic yanayoanza mwaka 2022