Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeipiga msasa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) kwa kuipatia mafunzo maalumu yenye malengo mbalimbali hasa katika kutetea maslahi ya Taifa.
Pamoja na mambo mengine, mafunzo hayo pia yatajikita katika masuala ya Itifaki, mawasiliano ya Kidiplomasia, usalama wa Kimtandao na Diplomasia ya Uchumi ili kuwajengea uwezo wabunge wa kamati hiyo katika kutekeleza majukumu yao ya Kamati na Bunge kikamilifu.
Akifungua mafunzo hayo Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amesema kupitia mafunzo hayo kamati itapata ujuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya Taifa, masuala ya Itifaki, mawasiliano ya Kidiplomasia, usalama wa Kimtandao na Diplomasia ya Uchumi.
“Ninayo furaha kuwajulisha kuwa mtapata fursa ya kuelimishwa juu ya mambo Uchumi wa Buluu, mada itakayotolewa na Wizara yenye dhamana ya usimamizi wa uchumi wa buluu kutoka Zanzibar ambayo imepiga hatua katika utekelezaji wake,” Amesema Balozi Mulamula.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Bw. Mussa Zungu amesema kamati anayoiongoza inafanya kazi kwa maslahi mapana ya nchi.
Mafunzo haya muhimu kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) yameandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Chuo cha Diplomasia na yatafanyika kuanzia tarehe 13 – 17 Septemba 2021 jijini Dar es Salaam