Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angeline Mabula, ametoa onyo kwa maafisa ardhi wanaorubuniwa na kuuza viwanja kwa ajili ya matumizi yaliyo kinyume cha mkakati mpango kabambe uliopangwa kwa fedha za ndani, uliowekwa na halmashauri na kusababisha migogoro ya ardhi isiyo ya lazima.
Amesema hayo wakati anazindua mpango kabambe wa mji wa Geita 2017-2037, kutokana na baadhi ya malengo yaliyoorodheshwa kutumia miaka mingi ya ukamilikaji.
”Pasiwepo na maombi ya kubadili mpango usio na tija kwa matashi ya mtu kwa urafiki wa mtu anawabadilishia mpango ambao nyie mmeumiza kichwa kuandaa halafu mtu mmoja anakaa anakimbiza vibali kwa kamishna, tunaomba mabadiliko haya tuingize hapa maadamu mmeshaweka simamieni” amesema Naibu waziri Mabula.
Naye mbunge wa Geita Constatine Kanyasu amesema mpango kabambe huo ni maandalizi ya kujiandaa kupanda kuwa Manispaa hiyo kutokana na mji huo kukua kwa kasi.
Kwa Upande wake Afisa mipango miji wa Halmashauri hiyo Matius Bujiku amesema mpango huo umezingatia maeneo yote maalumu kwaajili ya shughuli za kijamii, makazi viwanda biashara na miundombinu.
”Mpango huu utakuwa ni mpango wa miaka 20 wa uendelezaji wa mji wetu miji mingi ya hapa Tanzania imekuwa ikikua bila kufuata mpango wa jumla na hivyo kuzalisha makazi yasiyo pangwa, uaandaaji wa mpango huu umezingatia sheria na kanuni za mipango miji” amesema Bujiku.