Msafara wa Uongozi, Wachezaji na baadhi ya Mashabiki wa Young Africans uliokua nchini Nigeria umerejea nchini mchana leo Jumatatu (Septamba 20)majira ya mchana, baada ya kumaliza mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Awali dhidi ya Rivers United.
Young Africans ilicheza mchezo huo jana Jumapili (Septemba 19) mjini Port Hacourt na kuambulia kufungwa bao 1-0, na kujikuta ikitupwa nje ya michuano hiyo ya Afrika kwa jumla ya mabao 2-0.
Kurejea mapema kwa kikosi cha Young Africans kunatoa nafasi kwa benchi la ufundi la klabu hiyo kuanza maandalizi ya kuelekea mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii utakaowakutanisha dhidi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC.
Miamba hiyo itakutana kwenye mchezo huo ambao utaashiria kufunguliwa rasmi kwa msimu mpya wa 2021-22 siku ya Jumamosi (Septemba 25) Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.
Ikumbukwe kuwa mchezo wa Ngao ya Jamii huzikutanisha timu zilizotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho (ASFC), lakini kwa msimu huu imekua tofauti kwani Simba SC ndio Bingwa wa michuano yote hiyo.
Kanuni ya mshindi wa pili wa Ligi Kuu ambaye ni Young Africans kucheza mchezo huo wa Ngao ya Jamii imetumika, na sasa watani wa jadi watakutana kwa mara ya nne mfululizo mwaka huu 2021.