Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa serikali imeridhia madiwani kulipwa posho ya kila mwezi ili iwasaidie kuacha kuhangaika kukusanya fedha kwenye Halmashauri.
Ameyasema hayo leo Septemba 27, 2021 katika Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania-ALAT, wenye kauli mbiu ya ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu’ Jijini Dodoma.
Aidha Rais Samia amesema kuwa serikali itaendelea kuangalia maslahi ya madiwani na watendaji wengine kwenye Halmashauri nchini.
“Kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali imeridhia waheshimiwa madiwani kuanza kulipwa posho ya kila mwezi, na hii itasaidia kuacha kuhangaika na vile vijifedha vinavyokusanywa kule kujilipa kwenye maposho, posho yenu sasa imehakikishwa ipo,” Amesema Rais Samia.
Mkutano Mkuu Maalum wa Uchaguzi wa Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania-ALAT, ni mkutano wa kwanza kufanyika tangu kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka 2020.