Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Kenya zimeondoa vikwazo vya biashara 12 visivyo vya kikodi kati ya nchi hizo mbili.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kumalizia kwa Mkutano wa Sita wa Makatibu Wakuu wa Kamati ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Kenya uliofanyika Mombasa, Kenya kujadili na hatimaye kuondoa vikwazo vya biashara vilivyopo.
Hata hivyo hatua hiyo inafanya idadi ya vikwazo vilivyoondolewa kati ya Tanzania na Kenya kufikia 42 kutoka vikwazo 30 Taratibu za kuondoa vikwazo vilivyosalia zinaendelea.
Aidha Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara James Dotto, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Fatma Rajab na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban.
Katika Mkutano huo, Balozi Fatma Rajab amesisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo hivyo ikiwa ni njia ya kuimarisha biashara kwa nchi za Tanzania na Kenya pamoja na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo.
Naye, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Balozi John Simbachawene amesema kuendelea kuondoa vikwazo hivyo kunatoa fursa zaidi kwa Tanzania kufanya biashara na Kenya na kuwakaribisha wafanyabiashara wa Tanzania kuendelea kuchangamkia fursa za biashara zilizopo.