Wakati kikosi chao kikiwa kwenye maandalizi ya kuelekea mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22 dhidi ya Polisi Tanzania, Benchi la Ufundi la Azam FC limeendelea kusisitiza malengo ya kuufukuzia ubingwa wa Tanzani Bara.
Azam FC ilianza kwa kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union, imekua na mipango madhubuti kwa msimu huu, na tayari hilo limeonekana kutokana na usajili mkubwa waliofanya, ambao wanaamini utafanikisha lengo la kutwaa ubingwa.
Akizungumza kwa niaba ya benchi la ufundi la klabu hiyo linaloongozwa na Kocha Mkuu kutoka nchini Zambia George Lwandamina, Kocha Msaidizi Vivier Bahati, amesema dhamira yao kubwa ni kutaka kurejesha heshima ya kuwa mabingwa kama ilivyokua msimu wa 2013/14.
“Baada ya kuwa na mwanzo mzuri katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo timu yetu imefanikiwa kufuzu hatua ya kwanza, sasa ni muda wa kurejea kwenye mashindano mengine muhimu ambayo ni Ligi Kuu Bara.”
“Tumekuwa na maandalizi mazuri ya kabla ya msimu, pia tumefanya usajili bora kwa msimu huu wa 2021/22, malengo yetu makubwa ni kushinda ubingwa wa Ligi Kuu, kwa ubora wa kikosi chetu tunaamini hilo linawezekana.” amesema Vivier Bahati
Azam FC itapambana dhidi ya Polisi Tanzania, Jumamosi (Oktoba 2) katika Uwanja wa Ushirika mkoani Kilimanjaro.