Baada ya kuwasili salama katika jiji la Dodoma, Kikosi cha Mabingwa wa soka Tanzania bara Simba SC leo Alkhamis (Septemba 30) kimefanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Jamhuri jijini humo, tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu msimu huu 2021/22.

Simba SC itacheza dhidi ya Dodoma Jiji FC, katika mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa klabu hiyo, ambao wameonesha kusikitishwa na matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Biashara United Mara.

Kocha Msaidizi wa kikosi cha Mabingwa hao, Seleman Matola amesema wamekamilisha maandalizi yao kuelekea mchezo wa kesho Ijumaa (Oktoba Mosi), na wana matumaini makubwa ya kupambana na kupata ushindi wao wa kwanza msimu huu.

Matola amesema kuna baadhi ya wachezaji wao wataukosa mchezo huo wa kesho, akiwepo Shomari Kapombe, ambaye alishindwa kumaliza mchezo uliopita dhidi ya Biashara United Mara, kufuatia kupata majeraha ya kifundo cha mguu.

“Tumejipanga kupambana na kusaka matokeo katika mchezo wa kesho dhidi ya Dodoma Jiji FC, tumeyafanyia kazi makosa madogo madogo ambayo yalitukwamisha kwenye mchezo wetu wa kwanza dhidi ya Biashara United,”

“Hatupendi kuwakwaza mashabiki wetu, tunajua namna ya kuwafurahisha na tutahakikisha kesho tunawarudisha katika hali yao ya furaha ambayo wameizoa.” amesema Matola.

Dodoma Jiji FC walianza vizuri msimu mpya wa Ligi kuu kwa kuichakaza Ruvu Shooting kwa kuifunga bao moja kwa sifuri juzi Jumanne (Septamba 28), hivyo watahitaji kuendelea kufanya hivyo kwa mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC.

Hata hivyo Rekodi inawabana Dodoma Jiji FC, kwani tangu wamepanda daraja msimu wa 2019/20 hawajawahi kuifunga Simba SC, zaidi ya kuambulia visago katika michezo ya ligi kuu na Kombe la Shirikisho iliyochezwa nyumbani kwao na ugenini jijini Dar es salaam.

Mchezo mwingine wa mzunguuko wa pili wa Ligi kuu Tanzania Bara utakaochezwa kesho utashuhudia Biashara United Mara wakiendelea kuwa nyumbani mjini Musoma mkoani Mara, wakipambana dhidi ya Ruvu Shooting kutoka Mkoani Pwani.

Kitendawili serikali ya mseto Ujerumani kuteguliwa Oktoba?
Makubaliano ya Doha chanzo cha Afghanistan kuwa mikononi mwa Taliban