Meneja wa FC Barcelona Ronald Koeman amekiri kuwa na wakati mgumu wa kukilinda kibarua chake klabuni hapo, baada ya kikosi chake kukubali kisago cha mabao 3-0 dhidi ya Benfica, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya usiku wa kuamkia jana Alhamsi (Septemba 30).

Kichapo hicho kinaifanya FC Barcelona kupoteza michezo miwili mfululizo kwenye michuano hiyo ya Barani Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2000/01, huku ikiburuza mkia wa msimamo wa Kundi E.

Maneja huyo kutoka nchini Uholanzi ambaye aliwahi kuitumikia Barca kama mchezaji, amesema bado ana mazingira magumu ya kuendelea kusalia klabuni hapo, lakini hana budi kupambana ili kuiwezesha timu yake kufanya vizuri.

“Sijazungumzia hali jinsi ilivyo kwa timu,” amesema Koeman baada ya kupoteza kwa Benfica.

“Kila mmoja anajua matatizo ya sasa ya Barca. Huwezi kusema lolote kwenye timu ambayo sio ile ya miaka michache iliyopita. Kwangu mimi hili lipo wazi kama maji.”

“Siwezi kusema kuhusu majaliwa yangu. Nahisi napewa sapoti kubwa sana na wachezaji pamoja na hali jinsi ilivyo, lakini sijui nini klabu inafikiria.”

“Majaliwa yangu hayapo mikononi mwangu, na ndio maana sitaki kujibu swali lolote kuhusu majaliwa yangu. Tutaona nini kitakachotokea. Naikubali dunia ambayo sisi makocha tunaishi.” amesema

Wakati FC Barcelona ikifanya vibaya kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, upande wa Ligi Kuu ya Hispania inashika nafasi ya 6 ikiwa na alama 12, huku wapinzani wao Real Madrid wakiongoza msimamo huo kwa kufikisha alama 17.

Dodoma Jiji yaichimba mkwara Simba SC
Pep Guardiola akubali uwezo wa Donnaruma