Uongozi wa Young Africans umetangaza wazi kuwa mchezo wa kesho dhidi ha Geita Gold FC, wanaupa umuhimu mkubwa, kutokana na hitaji la alama tatu ambazo zitaendelea kuwaweka kwenye mazingira mazuri kwenye mchezo wa Ligi Kuu 2021/22.
Young Africans walianza vyema msimu huu kwa kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, juzi Jumatano (Septamba 29) katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.
Msemaji wa Young Africans Haji Sunday Ramadhan Manara amesema watapambana na Geita Gold FC kwa heshima licha ya kwamba imepanda daraja msimu huu.
Manara amesema baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambao walifanikiwa kuondoka na alama tatu kwa ushindi wa bao 1-0 wanaelekeza nguvu katika mchezo wa kesho dhidi ya Geita Gold FC.
“Tunakwenda hatua kwa hatua,hatutasema sana zaidi ya hamasa kwa watu wetu.Mchezo wa Kagera Sugar umepita, kwa sasa tunachoangalia ni mchezo dhidi ya Geita Gold.”
“Ni muhimu sana kwa kuwa ni mchezo wa kwanza nyumbani katika msimu huu. Haijalishi kwamba wamepanda daraja msimu huu lakini tunao wajibu wa kuwaheshimu kama timu ya ligi. Lakini wanapaswa kujua wanakuja kucheza na Yanga,” amesema Manara.
Kikosi cha Young Africans kilirejea jijini Dar es salaam jana Alhamis (Septamba 30), kikitokea mjini Bukoba mkoani Kagera, na leo kitafanya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo dhidi ya Geita Gold FC.
Geita Gold FC ilianza vibaya msimu, kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC iliyokua nyumbani mkoani Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu.