Kocha Msaidizi wa Geita Gold FC Fred Felix Minziro amesema kikosi chake kipo tayari kukabili Young Africa katika mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2021/22, kesho Jumamosi (Oktoba 02), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Minziro amesema wanaiheshimu Young Africans kwa ukongwe na uzoefu wao katika Ligi Kuu, lakini kikosi cha Geita Gold FC kimejipanga kupambana na kusaka matokeo kwenye Uwanja wa ugenini.
Amesema ugeni wao katika Ligi Kuu msimu huu, haupaswi kuwa kigezo cha kubezwa na wadau wa soka kuelekea mchezo dhidi ya Young Africans, na badala yake wanapaswa kutoa heshima kwa kila timu shiriki.
“Yanga ni timu kubwa na ina uzoefu wa kutosha katika Ligi Kuu, hilo tunalifahamu lakini halituzuii kwenda kupambana nao uwanjani,”
“Ligi Kuu ni mshindano magumu lakini Geita Gold FC tumejipanga kupambana na yoyote, ili kutimiza malengo ya kupata alama tatu muhimu zitakazotuwezesha kuwa sehemu ya timu zitakazomaliza katika nafasi nzuri mwishoni mwa msimu.” amesema Minziro
Geita Gold FC ilianza vibaya msimu, kwa kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC iliyokua nyumbani mkoani Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu.