Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imewapa maafisa saba wa Umoja wa Mataifa muda wa saa 72 kuondoka Ethiopia kwa kile ambacho serikali ya nchi hiyo imedai wamejiingiza katika mambo ya ndani ya nchi hiyo.

Aidha Serikali ya Ethiopia imechukua uamuzi wa kuwafukuza maafisa hao wa Umoja wa Mataifa baada ya wafanyakazi wa kutoa misaada kueleza juu ya hali ya maafa katika jimbo la Tigray inayotokana na kushindikana kupeleka misaada kwenye sehemu hiyo.

Marekani imesema itaiwekea vikwazo Ethiopia baada ya serikali ya nchi hiyo kuwafukuza maafisa saba wa mashirika ya kutoa misaada ya Umoja wa Mataifa ambao wanadaiwa kujihusisha na maswala ya ndani ya nchi hiyo.

Miongoni mwa maafisa hao saba wa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa wanoatakiwa kuondoka nchini Ethiopia ni pamoja na naibu mratibu wa misaada nchini humo Grant Leaty na mwakilishi wa shirika la watoto la UNICEF, Adele Khodr. 

Umoja wa Mataifa umesema hatua ya kuwafukuza maafisa wake kutoka nchini Ethiopia inahatarisha zaidi ufikishaji wa misaada ya kibinadamu katika mkoa wa Tigray ulio na watu wapatao milioni 6 na unaokumbwa na mgogoro kwa karibu mwaka mmoja sasa, huku msemaji msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephanie Tremblay, akisema Umoja wa Mataifa utaendelea kuziangazia shida zinazowakabili watu wa jimbo la Tigray.

Wazee waomba maboresho ya Afya
Makamu wa Rais wa Benki ya dunia kanda ya Afrika Mashariki amaliza ziara yake Nchini