Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Zuberi Homera amewatahadharisha wazee kujiepusha na mabinti ambao wanawanyemelea pindi tu wakipata viinua mgongo vyao baada ya kufanya kazi nzito kwa muda mrefu.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wazee katika Kijiji cha Ihahi Wilayani Mbarali mkoani humo.
“Mzee umefanya kazi kubwa, ukistaafu unakuta binti anakunyemelea, unamuacha bibi pekee yake unakwenda kuchukua binti mdogo wewe Babu ni Mzee lakini binti anakuita Bebi! Bebi!, ujue hapo anataka hela yako. Hakuoni kama wewe ni Bebi lakini pesa ile ndo Bebi. Anakuita Bebi si kwasababu ya ndevu na mvi ulizonazo, anakuita Bebi sababu ya pesa ulizonazo za kiinua mgongo baada ya kustaafu ualimu”. amesema RC Homera.
“Unamuacha Mzee mwenzako ambaye mlianza kuishi nae miaka ya 40 mmeishi pamoja, leo hii unamuacha na kwenda kuchukua Binti kadogodogo huko unakwenda kuishi nae. Matokeo yake unatengeza mazingira magumu kwa Bibi mwenzako na mwisho badala ya kuishi vizuri na yule Binti unaharibikiwa na kupoteza maisha”. Aliongeza zaidi Mhe Homera.
RC Homera ameendelea kuwaeleza wazee hao kwamba vijana kwasasa ni watukutu sana maana wakimng’ang’ania Mzee hawamwachi mpaka anapoteza maisha.