Viongozi wa Serikali wametakiwa kuwatumikia wananchi na kuleta maendeleo huku wakuu wa mikoa wakionywa juu ya swala la rushwa na kugeuka miungu watu.

Hayo yamesemwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan leo Oktoba 11,2021 wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Mjema.

“Uongozi ni dhamana siyo zawadi..tunategemea viongozi mtakuwa mfano, sitegemei kuona mkuu wa mkoa anaingia kwenye vitendo vya rushwa, sitegemei kuona wakuu wa mikoa mnakuwa Miungu watu huko mliko, mpo kule kutumikia watu, siyo watu wawatumikie nyie. Naomba mkafanye kazi tulizowatuma,” amesema Rais Samia.

“Samia Suluhu ninakotoka hakuna makabila, mimi sina kabila, mwalimu Nyerere hakuwa na kabila.. kwenye utendaji wangu wa kazi ukilikoroga nakutumbua bila kuangalia kabila, anayekosea nitamuondoa, sipangi kwa kuangalia kabila, napanga kwa uwezo wake ili kwenda kusaidia wananchi kuleta maendeleo.

Mimi kwenye utendaji wangu wa kazi sina Kabila, uwe Mmakonde uwe mnani ukikosea kwenye kazi Mimi na wewe wala sitokufumbia jicho, sasa kama umetoka ulikotoka ukitumbuliwa ‘Mimi wa Kabila fulani’ hiyo sumu mnaipeleka sana, naomba isimame.”,amesema Rais Samia.

Dulla Mbabe: Sitapanda ulingoni hadi 2022
Ushiriki wa Afrika Kombe la Dunia 2022