Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama, amesema jumla ya miradi ya maendeleo 1,067 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.2 katika sekta mbalimbali imezinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi nchini kote, wakati wa mbio maalum za Mwenge wa Uhuru zilizokimbizwa kwa takribani miezi mitano.
Waziri Mhagama ameyasema hayo katika uwanja wa Magufuli wilayani Chato mkoani Geita wakati wa kilele cha mbio maalum za Mwenge wa Uhuru, kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kilele cha wiki ya Vijana kitaifa.
Amesema wakati wa mbio zake, Mwenge wa Uhuru umekataa kuzindua ama kuweka mawe ya msingi kwenye miradi 41 iliyopo katika wilaya 38 nchini, kutokana na miradi hiyo kuwa na dosari mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa harufu ya rushwa kwenye miradi hiyo.
Aidha Waziri Mhagama amesema tayari Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imekabidhiwa taarifa za miradi hiyo kwa ajili ya kufanya uchunguzi, na wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu watachukuliwa hatua za kisheria.
Kauli mbiu ya mbio maalum za Mwenye wa Uhuru kwa mwaka huu uliokimbizwa kwa siku 150 bila kupumzika katika wilaya 150 za kiutawala ni TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu, Itumie kwa usahihi na Uwajibikaji.
Sambamba na hayo yote Waziri Mhagama ametumia sherehe hizo kutangaza kuwa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022 utafanyika mkoani Njombe na kilele cha mbio hizo, kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wiki ya Taifa ya Vijana kitakuwa mkoani Kagera.