Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, limeruhusu mashabiki kuingia uwanjani kwenye mechi za klabu za Tanzania za michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Wakati Biashara United watakuwa wenyeji wa Al Ahly Tripoli ya Libya jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa, Azam FC watawaalika Pyramids ya Misri kesho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi katika mechi za kwanza Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho.
Na mabingwa wa Tanzania, Simba SC wataanzia ugenini Jumapili dhidi ya Jwaneng Galaxy Jijini Gaborone, Botswana kabla ya kumalizia nyumbani wiki ijayo.
Ikumbukwe michezo ya hatua ya awali yote iliyoihusisha Azam FC, Biashara United na Young Africans waliotolewa na Rivers United ya Nigeria katika Ligi ya Mabingwa haikuwa na watazamaji kwa zuio la ‘CAF’ ambayo ilizuia watazamaji hadi kwenye michezo ya timu ya Taifa nchini.