Aliyekua Mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya na wenzake wamehukumiwa Kifungo cha Miaka 30 Jela kwa kosa la Unyang’anyi wa kutumia Silaha.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Arusha, Odira Amworo amesema kuwa ameridhika na mashtaka dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Sabaya na wenzake wawili na kuwatia hatiani.
Hukumu ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha iliyokuwa ikimkabili Sabaya imesomwa leo Ijumaa Oktoba 15, 2021 na Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo.
Wakili wa Serikali, Felix Kwetukia aliweka wazi kuwa Jamhuri ipo tayari kupokea hukumu huku upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Moses Mahuna, Silvester Kahunduka na Wakili Fridolin Germelo nao walisema wapo tayari kusikiliza hukumu hiyo.
Hakimu Omworo amesema kuwa imethibitika mshitakiwa wa kwanza alikuwa na bastola ndani na nje kulikuwa na watu wawili wenye silaha. Hivyo, hakuna shaka duka la shahidi wa kwanza lilivamiwa na watu wenye silaha na lilikuwa chini ya watu wenye silaha.
Sabaya na wenzake walifikishwa mahakamani leo saa 3:05 asubuhi, kwa ajili ya hukumu ambapo Oktoba 1 2021 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Amalia Mushi aliahirisha hukumu hiyo kwa maelezo ya kutokamilisha kuandika hukumu hiyo.
Sabaya na wenzake wamehukumiwa baada kesi yao kusikilizwa kwa muda wa miezi 6 tangu ashitakiwe kwa makosa hayo.
Hapo awali Sabaya alikutwa na Hatia na kupewa muda wa kujitetea kabla ya hukumu na katika utetezi wake alisema alikua anatekeleza maagizo kutoka kwa Mamlaka iliyomteua huku akiomba kupunguziwa Adhabu kwa kuwa Ana mchumba anataka kuoa.