Kocha wa Young Africans, Nesreddine Nabi amemaliza tofauti zake na mshambuliaji wake Saido Ntibazonkiza akisema tayari kila kitu kipo sawa kisha akampa kazi moja tu.
Nabi amesema hana tatizo lolote na Saido kwa sasa na kwamba kila kitu kimekuwa sawa baada ya mshambuliaji huyo kuwa nje ya kikosi hicho kwa muda.
Nabi amesema amefanya kikao kirefu na mshambuliaji huyo mkongwe na kila kitu sasa kipo sawa lakini pia amempa nafasi ya raia huyo wa Burundi kujieleza mbele ya wachezaji wenzake akiwa kama mchezaji mzoefu.
“Sina matatizo yoyote sasa na Saido, yeye ni sehemu ya hii timu na tuko naye ingawa hakusafiri. Kila kitu kimemalizika, tunatakiwa kuwa na nidhamu sawa kwa kila mmoja katika timu hii,” amesema Nabi na kuongeza
“Nimezungumza na Saido na tumekubaliana lakini pia aliongea na wenzake wote wameelewana, sasa yuko na sisi katika safari moja ingawa tulimuacha katika safari hii ya Songea.
“Kazi aliyonayo Saido ni kupigania nafasi yake kwenye timu, nikiona anaimarika kama ninavyotaka nitampa nafasi, sina tatizo na mchezaji ambaye naona anaweza kusaidia hii timu, tunahitaji mafanikio na kazi hiyo itafanywa na sisi makocha na wachezaji,” amesema.
Saido hajaonekana katika michezo yote mitatu ya kwanza msimu huu huku ikitajwa kwamba mshambuliaji huyo alikuwa na tofauti na kocha Nabi.