Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO) imetoa wito kwa viongozi wa mikoa nchini kujenga utaratibu wa kufanya matamasha ya ulaji nyama ili kuhamasisha wananchi kuongeza wigo wa kula nyama ili kujenga afya zao na kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini.
Hayo yamesemwa na Meneja Masoko wa NARCO Immanuel Mnzava wakati wa tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival lilioandaliwa na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Mkoani Rukwa likienda sambamba na uanzishaji wa mnada katika Kata ya Pito, Kijiji cha Katumba Azimio.
Akizungumza juu ya tamasha hilo Mnzava amesema NARCO kama mdau mwalikwa kwenye tamasha hilo inahamasisha ulaji wa nyama na hasa nyama ya Kongwa Beef inayozalishwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO) ambayo ina ranchi 14 nchini ikiwemo Ranchi ya Kalambo iliyoko Mkoani Rukwa.
Amesema uhamasishaji huu unafanyika ili kuongeza ulaji wa nyama nchini kwa kuwa kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ulaji wa nyama nchini kwa mtu mmoja bado uko chini ambapo ni wastani wa Kilogramu 15 kwa mwaka tofauti na pendekezo la dunia la ulaji wa Kilogramu 50 kwa mwaka.
“Ulaji unaopendekezwa duniani ni Kilogramu 50 kwa mwaka. Kwa hiyo kwa wastani kila mwananchi ili afikie viwango vya ulaji nyama vinavyopendekezwa duniani anadaiwa kuongeza Kilogramu 35 ili afikishe kilo 50 kwa mwaka, ili kufikia viwango hivyo, Tanzania inadaiwa wastani wa tani za nyama 2,100,000 kwa mwaka.” Amesema Mnzava.
Aidha, amesema kuwa lengo la matamasha la ulaji nyama nchini yataongeza soko la ndani la bidhaa za mifugo na mazao yake na kutoa fursa kwa wananchi kufurahia rasilimali zinazozalishwa nchini katika sekta ya mifugo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Bw. Joseph Mkirikiti akizungumza juu ya tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival amesema ni moja ya vyanzo vya mapato na matamasha hayo yatafungua fursa ya utalii wa ndani nchini.
Amebainisha pia uwepo wa NARCO ni sehemu ya kuliongezea pia thamani zao la ngozi kwa kuwa ulaji wa nyama ukiongezeka utasababisha pia uwepo wa ngozi za kutosha katika matumizi ya viwandani pamoja na chakula.
Tamasha la Sumbawanga litafanyika kila mwisho wa wiki sambamba na mnada katika Kata ya Pito, Kijiji cha Katumba Azimio.