Idadi ya vifo vinavyotokana na kuanguka kwa jengo lenye ghorofa 21 lililokuwa kwenye hatua za ujenzi katika jiji la Lagos nchini Nigeria imeongezeka hadi kufikia watu 16, kwa mujibu wa ripoti ya Serikali.
Jengo hilo lilianguka Jumatatu wiki hii ambapo jitihada za kuwaokoa majeruhi zinaendelea usiku na mchana. Ingawa haijaelezwa kwa kina chanzo cha kuanguka kwa jengo hilo, mvua kubwa iliyonyesha usiku katika jiji hilo inatajwa kuwa sehemu ya sababu.
“Tumepata miili zaidi. Idadi ya vifo sasa imeongezeka hadi watu 16, na watu 9 walitolewa kwenye vifusi wakiwa hai,” amesema Ibrahim Farinloye kutoka Kitengo cha Taifa cha Usimamizi wa Matukio ya Dharura.
Ameongeza kuwa mapema jana, waokoaji walikuwa wanaweza kuzungumza na baadhi ya majeruhi waliokuwa wamenasa kwenye vifusi.
Serikali imeeleza kuwa mmiliki wa jengo hilo aliongeza ghorofa sita zaidi ya idadi iliyokuwa imepata kibali. Hatua inayotajwa kuwa ni mchezo mchafu uliozidisha uzito usiostahili.
“Niko hapa, naona vifaa alivyotumia ni vya hali ya chini na vibovu. Alipewa kibali cha kujenga ghorofa 15 lakini alijenga 21,” alisema Gbolahan Oki, Meneja Mkuu wa Wakala wa Majengo wa Jiji la Lagos.
Serikali ya jiji la Lagos imemsimamisha kazi Mkuu wa Majenzi wa jiji hilo na imeanzisha uchunguzi huru wa kina kufahamu chanzo halisi cha tukio hilo.