Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema tozo nyingi katika sekta ya uvuvi ambazo zipo chini ya wizara tayari zimeboreshwa na nyingine kuondolewa ili kuweka mazingira mazuri zaidi ya kufanya kazi kwa wadau wa uvuvi nchini.
Dkt. Tamatamah amesema hayo katika Mwalo wa Ihale uliopo Wilaya ya Busega, Mkoani Simiyu, wakati akikagua ujenzi wa sehemu ya kushushia samaki, kuhifadhia, kuuzia pamoja na ofisi ya Kikundi cha Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika mwalo huo.
Ambapo amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na wizara zingine pamoja na halmashauri za wilaya kote nchini zinaendelea kuangalia tozo za uvuvi ambazo siyo rafiki kwa wadau wa uvuvi.
Amesema nia ya serikali ni kuondoa vikwazo vya biashara na utekelezaji wa agizo kutoka katika mamlaka ya juu ya serikali katika mwaka huu wa fedha 2021/22 wa kuondoa tozo ambazo zinakwamisha maendeleoa ya sekta mbalimbali nchini.
“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Samia Suluhu Hassan alisema katika wizara zote ziangalie upya tozo ambazo katika ile sekta zipo kwa kushirikiana na halmashauri kwa mfano sisi wizara ambazo zipo chini ya wizara nyingi tumezipunguza, kila tunapopita katika halmashauri tunawaambia pamoja na wizara zingine juu ya tozo zinazohusu sekta ya uvuvi.” Amesema Dkt. Tamatamah
Awali akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Busega Mkoani Simiyu Gabriel Zacharia amumueleza Dkt. Tamatamah juu ya uwepo wa tozo ambazo wadau wa uvuvi wamekuwa wakizilalamikia ikiwemo ambayo inatozwa kwa thamani ya dola za kimarekani.