RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa daraja na amani na mtu anayependa maridhiano ya kisiasa badala ya malumbano na vurugu kama walivyo baadhi ya wanasiasa.
Rais Samia amesema hayo leo Ijumaa, Novemba 1, 2021 wakati akihutubia kwenye ufunguzi wa mkutano wa maadhimisho ya maisha ya Maalim Seif ambaye alifariki dunia Februari 17, 2021.
Amesema kwamba hata kama imetokea Maalim Seif akavuliwa vyeo vyote alivyowahi kushika lakini bado atabaki kuwa ni mwalimu wa watu kwa sababu watu wengi walimpenda, kumtumaini na kumheshimu.
“Nimesimama mikutano mingi kuongea na mingine ya kimataifa. Lakini sijaona ugumu kama naouona katika mkutano huu. Enzi za uhai wake, Maalim Seif alikuwa ni makutano ya watu, alikuwa ni kiongozi wa watu na alitokana na watu na watu walimshiba. Na huyo ndio Maalim Seif na watu kukutana leo kumkumbuka sio jambo la ajabu,” Amesema Rais Samia.
“Pamoja na kwamba Maalim Seif alifanya kazi ya ualimu hata kuitwa maalim, umaalim wake ni wa kipekee kutokana na kuwa hakuwa tu mwalimu wa wanafunzi bali pia alikuwa ni mwalimu wa watu. Maalim Seif alikuwa na uthibiti wa msimamo wake na alikuwa na utayari wa maridhiano hata pale unapotokea msigano. Na amefanya kazi hii ndani ya chama chake na katika vyama vingine.