Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire ameanza kutema cheche kuelekea mchezo wa mzunguuko watano, ambao utawakutanisha na Mabingwa watetezi Simba SC.
Ruvu Shooting watakua wenyeji wa mchezo huo, utakaopigwa Ijumaa (Novemba 19) Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Masau amesema ubora wa kikosi chao unaendelea kuwa matumaini ya kupambana na yoyote katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, na wakapata matokeo ya alama tatu.
Amesema kutokana na kutumia kikosi kazi chenye wachezaji wazawa, imekua silaha yao kubwa kila msimu lakini kwa msimu huu wamejizatiti zaidi kupambana hadi tone la mwisho.
“Tuna wachezaji wazuri ambao wana uwezo mkubwa na kila mchezaji malengo yake ni kuona timu inapata ushindi.
“Mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi kwa kuwa kila kitu kinawezekana na kikubwa ni kupata matokeo mazuri.”
Hata hivyo Ruvu Shooting wanajiandaa kupambana na Bingwa Mtetezi, huku wakiwa na jeraha la kufungwa na Young Africans mabao 3-1, siku chache kabla ya kikosi cha Taifa Stars hakijaingia kambini kujiandaa kupambana na DR Congo.
Simba SC wao wana kumbukumbu ya kuifunga Namungo FC bao 1-0, huku wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 11 na wenyeji wao watarajiwa Ruvu Shooting wapo nafasi ya 10 wakiwa na alama 6.