Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua mkakati wa Taifa wa kuzuia magonjwa yasiyoambukiza utakaosaidia kutoa elimu juu ya njia za kupambana dhidi ya magonjwa hayo zikiwemo kufanya mazoezi, kula vyakula vya gharama nafuu visivyochangia kuleta magonjwa hayo kama inavyoelekezwa na wataalamu, kuepuka matumizi ya vileo kupita kiasi na mambo mengine yanayoelimishwa na wataalamu.
Uzinduzi huo umefanywa leo Jijini Arusha na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima na kuhudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulika na masuala ya Afya OR TAMISEMI Dkt. Grace Magembe pamoja na Wadau kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali na zisizo za Serikali.
Dkt. Gwajima amesema, Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 Duniani vilivyotokea mwaka 2016, hii ni kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za Mwaka 2016.
“Takwimu za Shirika la Afya Duniani za Mwaka 2016 zinaonesha kuwa Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 Duniani vilivyotokea mwaka 2016. Hali hii inatishia ustawi wa maendeleo ya mwanadamu.” Amesema Dkt. Gwajima.
Amesema magonjwa yasioambukiza yalikuwa yanachangia asilimia 20 tu miaka ya 90 lakini kwa sasa yanachangia asilimia 33 na inakadiriwa yanaweza kufikia hadi asilimia 40 katika baadhi ya maeneo nchini, alisisitiza.
Hata hivyo Dkt. Gwajima amesema kuwa, jambo linalotia hofu ni kuwa katika jamii zetu magonjwa haya yanaanza mapema zaidi na hivyo kuzorotesha nguvu kazi na kusababisha vifo katika umri chini ya miaka 60.
Aidha, ameweka wazi kuwa, Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka 20, kuanzia mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa haya Duniani zitafikia Dola za Marekani trilioni 47, fedha ambazo zingeweza kutumika kupunguza umaskini kwa watu bilioni 2.5 kwa miaka 50…