Wakati baadhi ya mashabiki wa muziki wa bongo fleva wakiendelea kuomba siku moja walau mara moja itokee msanii Diamond Platnumz kurejea kwenye maelewano mazuri na Harmonize ikiwezekana kufanya wimbo wa pamoja kama ishara ya amani kati yao kama ilivyokuwa awali
Wawili hao wameendelea kudhihirisha kuwa hiyo kwasasa bado ni ndoto ya Ally Nacha kutokana na namna ambavyo wamekuwa wakirushiana maneno makali kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii yenye kuashiria uwepo wa chuki kubwa miongoni mwao yenye kuyatafuna matumaini ya kurejea kwa maelewa ya wakali hao wa muziki nchini.
Kasheshe jipya limezuka Usiku wa kuamkia leo Nov 15, mwaka 2021. Kufuatia maneno aliyoyaandika msanii Diamond platnumz baada ya Rayvanny kufanikiwa kuingia kwenye rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kutoka barani Afrika kupata nafasi ya kutumbuiza kwenye tamasha maalumu wakati wa utolewaji wa tuzo za MTV EMA 2021 huko Budapest, Hungary.
Diamond kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram aliweka kipande cha video chenye kumuonyesha rayvanny akitumbuiza kwenye jukwaa hilo kuwa akiwa na msanii Juan Luis maarufu ‘Maluma’ kutoka nchini Columbia na kisha kuandika maneno yenye kusomeka.
“The first African artist to perfom #MTVEMA Rayvanny Chui…..Ninawakumbusha msanii wa kwanza Africa Kuperform MTV EMA anatokea Tanzania, mkoa wa Wasafi na sasa ni Rais wa Next Level Music, Mh Rayvanny…..Vijana wenzangu tujifunzeni kuwa na nidhamu na fadhila ili Sanaa zetu zitufikishe mbali zaidi na tusiishie kwenye Mihadarati”. Aliandika Diamond.
Ujumbe huo wa Diamond umehusishwa moja kwa moja na kijembe kwa msanii Harmonize ambaye naye masaa saba baadaye, aliamua kuandika ujumbe mrefu kwenye ukurasa wake wa Instagram (Insta story) ambao pia umetafsiriwa kama majibu ya kile ambacho Diamond amekituma kama dongo au kijembe kwake.
“Vijana ni vyema kujifunza, ukimsaidia mtu sio lazima kudai fadhila, maana kama ndio hivyo basi Tanzania yote inanidai pia, ukishapokea mamilioni ya shilingi 600M, ukishavutia unga yakishakaribia kuisha ni vyema kuyauliza au kuyadai fadhila….!!!
Pia vijana jifunzeni kutofautisha kipi ni hatari kati ya mihadarati na huo unga unaowakondesha…!!! Vijana jitahidini kutofautisha kati ya wewe mwenye miaka 11 na mwenye miaka 6 umefika wapi maana Bar ni zile zile, Kitchen part ni zile zile huku USA.
Licha ya kuvimba kote mkiwa kwenye jiji la mama Samia…!!! Vijana ni vyema kuwalipa wakina mama Levo waendelee kutukana watu unaotaka wakuheshimu huku ukiamini watakufa kimuziki bila kujua unawalipia Promotion.
Vijana jifunze kuposti msanii wako akitoa wimbo sio kuumia kwa kutolewa kwenye kolabo na sio kutafuta pakutokea kupitia kijana mwenzio sio vizuri kaka”, aliandika Harmonize.
Ambapo muda mfupi baadaye aliongeza posti nyingine yenye kushutumu kuhusu kuwepo kwa mchezo mchafu unaofanya kwenye upande wa tuzo za wasanii barani Afrika ” Mkishakosa tuzo zisizo nunulika msikimbilie Ngada haraka, rudini Studio subirieni Afrima” aliongeza.
Uhasama mkubwa kati ya Diamond platnumz na Harmonize ulijidhihirisha wazi mnamo 2019, punde baada ya msanii Harmonize kujitoa WCB Wasafi, Label ya Muziki inayomulikiwa na msanii Diamond Platnumz.
Harmonize kwa sasa ni mmiliki wa Label yake mwenyewe iitwayo Konde Music Worldwide.