Mwanamitindo na mjasiriamali maarufu nchini Flaviana Matata amefunguka mazito aliyopitia kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuachana na mume wake mnamo mwaka 2019.
Matata amefunguka ya moyoni na kuelekeza ujumbe wake kwa baadhi ya watu ambao wamekuwa wakiwaangushia mzigo wa lawama na kuwadhihaki wanawake pekee inapotokea ndoa zao kuvunjika.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram Flaviana ameandika.
“Hakuna anayefunga ndoa ili mwisho wa siku aishie kwenye kupewa talaka, nikiongea kwa kutumia uzoefu wangu, mwaka 2019 nilitalikiana lakini mitandao haikuniacha hata nipumue, ilikuwa ni kama nimefanya mauaji, kwa sasa nipo kwenye hali nzuri na nimepona, nawashukuru watu wangu wachache wa karibu kwa kuwa na mimi katika kipindi chote, ni kwa vile baadhi yetu tumechagua kuficha maumivu yetu kwenye hadhira”. Aliandika Matata.
Licha kudhihirisha namna alivyopitia wakati mgumu, Flaviana Matata aliongeza kwa kugusia kitu alichojigunza kuhusu mitandao kipitia tukio hilo;
“Kwenye Mtandao kunaweza kuwa na ukatili na hii inapelekea kutengeneza ugumu kwa watu kuongelea matatizo yao isipokuwa kwa watu wao wa karibu pekee, hatushiriki kumsaidia mtu yeyote kwa kumdhihaki pale ndoa yake inaposhindwa kuendelea mbele, na hii ndio sababu ya kwanini watu wengi wanabaki kwenye ndoa zenye unyanyasaji na uonevu.” Aliongeza.
Flaviana ameyasema hayo kufuatia alichokiona kwenye mahojiano aliyoyafanya Oprah Winfrey na mwimbaji Adele yaliyojawa na mengi kuhusu maisha ya mwanamuziki huyo na mapitio yake maishani.