Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Afya na watafiti mbalimbali kujikita katika kutambua sababu za kuongezeka kwa matatizo ya Saratani katika mikoa ya kanda ya ziwa.
Rais Samia ameyasema hayo katika maadhimisho ya miaka 50 ya hospitali ya Rufaa ya kanda ya ziwa Bugando, akisema ndani ya miaka mitatu uliyopita wagonjwa wengi ni wanawake kwa kiasi cha kufikia elfu mbili kila mwaka.
Rais Samia pia amewataka wahusika wakuu wa hospitali kupitia fedha za IMF zilizotolewa, wafanye manunuzi ya vifaa kwa kuzingatia ubora na kuangalia viwanda ambavyo vinaweka udhibiti wa vifaa.
Nae Waziri wa Afya Dk Dorothy Gwajima amesema Fedha za IMF zimesaidia kuleta maendeleo katika hospitali hiyo ikiwemo mashine ya MRI ambayo imezinduliwa na Rais Samia na amewataka wananchi wote kujiunga na Bima ya Afya ili wapate huduma kwa urahisi.
Awali akitoa maelezo kwa mgeni rasmi Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando DK Fabian Mgasa amesema hospitali kupitia maboresho mengi yaliyofanywa na Serikali imefanikiwa kugundua mdudu mpya anaesumbua kwa afya za watoto na kwa sasa wanatibu magonjwa ya watoto kwa urahisi.
Hospitali ya Rufaa ya Bugando ni ya pili kwa ukubwa ikitanguliwa na Hospitali ya Muhimbili na ilizinduliwa rasmi na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tarehe 3 Novemba 1971 na ilikua chini ya kanisa katoliki ikiitwa Mwanza Hospitali, na ilipofika mwaka 1972 ilichukuliwa na serikali lakini baadae miaka 13 mbele serikali ilirejesha umiliki kwa baraza la Maaskofu kwa makubaliano maalum ya kuiendesha.