Waziri wa kilimo Profesa Adolf Mkenda, amewataka wakala wa mbegu nchini (ASA) kuhakikisha mbegu za alizeti zinawafikia wakulima kwa wakati kwa lengo la kuongeza mapambano katika kukabilina na tatizo la uhaba wa mafuta ya kula nchini kila mwaka.
Profesa Mkenda amesema hayo wakati wa makabidhiano ya mbegu hizo mjini Singida, ambapo amesema Tanzania hutumia zaidi ya shilingi Bilioni 450/- kila mwaka kugharamia mafuta ya kula kutoka nje ya nchi, ambazo zikiokolewa, zitatumika kutekeleza miradi mingine mbalimbali ya maendeleo.
Naye, mtendaji mkuu wa wakala wa mbegu nchini (ASA) Dk. Sophia Kashenge, amesema ili kwenda sawa na msimu wa mvua, Wizara ya Kilimo inafanya mazungumzo na wizara ya ulinzi, kuhakikisha magari ya jeshi la Wananchi (JWTZ), yanatumika kusambaza mbegu hizo ili ziwafikie wakulima kwa wakati.
Dk. Kashenge amefafanua kuwa katika uzinduzi wa ugawaji wa tani 52 za mbegu hizo, ni kwa ajili ya wilaya ya Mkalama na Iramba,ambazo zimewakilisha mikoa mitatu ya kimkakati kwa kilimo cha alizeti, yaani Singida, Simiyu na Dodoma.
Naye mkuu wa mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge, akatumia fursa hiyo kuomba mbegu zaidi, zitakazoweza kutosheleza mahitaji ya mkoa huo, ambazo ni tani 465.2, lakini mpaka sasa tayari serikali ya mkoa imefanikiwa kupokea tani 279.9.
“Mheshimiwa waziri nakuamini sana katika kutekeleza majukumu yako, mpaka sasa umefanya kazi kubwa sana, lakini ombi letu lilikuwa ni tani 465.2 za mbegu, kama umefanikiwa kutuletea tani 279.9…naamini kwa kiasi kilichobaki hakiwezi kukushinda,”alisema Dk. Mahenge.
Kwa upande wake mwakilishi wa mfuko wa maendeleo ya kilimo nchini (IFAD) Jaquleen Machagu, amesema kuwa mbegu hizo ni katika kuwasaidia wakulima walioathiriwa na tatizo la UVICO-19.