Katibu wa Geita Gold FC Revinus Ntare amethibitisha taarifa za klabu hiyo kumsajili Mshambuliaji Ditram Nchini ‘Duma’ ambaye Desemba 15 atakuwa mchezaji huru, akiachana na klabu ya Young Africans.
‘Duma’ anaondoka Young Africans, kufuatia mkataba wake kumalizika, huku akishindwa kujihakikishia nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
Ntare amesema wamekamilisha mpango wa kumsajili Mshambuliaji huyo, na rasmi ataanza kuonekana kwenye kikos cha Geita Gold FC, baada ya kufunguliwa kwa Dirisha Dogo la usajili Desemba 15.
Amesema Uongozi wa Geita Gold FC unaamini uzoefu wa Nchimbi katika Ligi Kuu utaongeza chachu kwenye kikosi chao, na hatimaye kufikia lengo la kupambana vilivyo msimu huu.
“Ni kweli tumemsajili Nchimbi ila atajiunga na timu baada ya mwezi mmoja mara dirisha dogo likifunguliwa, naamini ataleta nguvu mpya ndani ya Geita kuichangamsha safu ya ushambuliaji,” amesema Ntare
Kabla ya taarifa za Nchimbi kusajiliwa Geita Gold FC kuthibitishwa, Mshambuliaji huyo alihusishwa na mpango wa kuwaniwa na klabu za Mtibwa Sugar, Namungo FC na Polisi Tanzania FC.