Rais wa Uganda Yoweri Museveni anasema kundi la waasi, Allied Democratic Forces linastahili kujisalimisha huku akisisitiza kuwa serikali yake imejitolea kukabiliana na ugaidi.
Katika hotuba liliyorushwa moja kwa moja kwenye televisheni siku tano baada ya shambulio dhidi ya mji mkuu wa Kampala, Museveni alisema ADF wamejiamini sana kwa sababu wanaweza kutembea huru katika kambi za kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na wanajishughulisha na uchimbaji madini na biashara za mbao.
Hata hivyo amesema kuwa Uganda itaendelea kuwasaka wanachama wa kundi hilo na kuongeza kuwa ni vyema wale ambao hawajasalimisha silaha zao wafanye hivyo.
Islamic State, IS lilidai kuhusika na shambulio la Jumanne ambalo lilisababisha vifo vya watu wanne na kuwajeruhi wengine zaidi ya 30.
Museveni amesema kuwa ADF sasa wamegeukia vitendo vya ugaidi katika maeneo ya mijini baada ya kushindwa katika eneo la Rwenzori na vijijini 2007..
Rais Museveni kwa sasa anafanya mazungumzo, na Rais DRC, Felix Tshiekedi juu ya uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa Uganda mashariki mwa Kongo kupambana na kundi la waasi.