Ni takribani wiki mbili zimepita tangu ilipotolewa taarifa rasmi ya kupata na kurejea kufanya kazi pamoja kwa wasanii mapacha Peter Okoye na Paul Okoye maarufu P-Square waliokuwa kwenye ugomvi mzito kwa takribani miaka mitano.
Muda mfupi baada ya kuzika tofauti zao wakali hao kutoka nchini Nigeria walitangaza ujio wa show yao ya kwanza tangu kurejea kwenye muziki kama kundi ambayo imefanyika mapema usiku wa kuamkia leo Nov. 28, 2021 huko Sierra Leon.
Kupitia akaunti za kurasa zao za mitandao ya kijamii Peter na Paul wameweka wazi kushtushwa na ukubwa wa mapokezi ya mashabiki wa muziki nchini humo, ambao wamejitokeza kwa wingi kuwashuhudia wasanii hao machachari baada ya muda mrefu kutoonekana wakiwa pamoja jukwaani.
Licha ya kutokuwepo kwenye tasnia ya muziki kama kundi tangu mwaka 2017, wawili hao waliendelea kufanya kazi kwa mfumo wa kila mmoja akijitegemea kivyake, kutokana na ugomvi uliotokea baina yao, unaodaiwa kusababishwa na mgogoro wa maslahi ya kikazi huku upande wa pili chanzo kikitajwa kuwa ni maswala ya kifamilia yalichagizwa na wake zao kutokuwa na maelewano mazuri.