Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, amewataka watumishi wa umma nchini kuacha kiburi na majivuno pindi wanapotoa huduma kwa wananchi kwani mishahara wanayolipwa na Serikali inatokana na kodi za wananchi.

Waziri Mchengerwa ametoa wito huo kwa watumishi wa umma nchini, wakati akifungua semina ya viongozi wa Matawi ya TUGHE na Waajiri inayofanyika jijini Arusha. 

Mchengerwa amesema, watumishi wa umma wanapaswa kuwahudumia wananchi ipasavyo kama ambavyo wao wanatamani kuhudumiwa na Serikali.

“Baadhi yetu, kuna vitendo tunavifanya ambavyo haviwapendezi wananchi tunapowahudumia, hivyo tuhakikishe tunatoa huduma bora kama ambavyo sisi tunavyoitaka Serikali ituhudumie,” amesema Mchengerwa.

Mchengerwa amesema kuwa, fikra na maono ya Rais wa Awamu ya Sita, Mhe. Samia Suluhu Hassan ndio fikra na maono ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hivyo Watumishi wa Umma tunapaswa kuishi kwa vitendo fikra na maono hayo ili kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha amewataka Watumishi wote wa Umma nchini kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi aliyonayo anafanya kazi kwa bidii na weledi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Balozi Mulamula akutana na Waziri wa China Nchini Senegal
Minziro: Tumejiandaa kuikabili Simba SC