Novemba 29, mwaka 2021, mtandao wa Apple Music ulitangaza rasmi majina ya washindi wa tuzo za Apple Music zitolewazo kila mwaka.
Katika tangazo hilo nyota wa muziki kutoka nchini Nigeria Wizkid alitangazwa kuwa msanii bora wa mwaka barani Afrika ‘Apple Music Artist of the Year’, huku msanii The Weekend kutoka nchini Marekani akitangazwa kuwa Msanii Bora wa Mwaka Duniani kote.
Kipengele cha Wizkid kinasomeka, “Mwimbaji na mtunzi Wizkid ni mmoja wa wasanii wakubwa barani Afrika, ambaye amefanya kazi na Drake, Skepta na Chris Brown, miongoni mwa wasanii wengi wakubwa duniani.
Mwanamuziki huyo wa Nigeria alipata mafanikio ya kikanda mnamo mwaka 2011 kupitia wimbo wake maarufu uitwao ‘Holla at Your Boy’, ambao unapatikana kwenye albamu yake ya kwanza iitwayo “Superstar.”
Wizkid alianza kuvuma na kuupenyeza muziki wake duniani kote kuanzia mwaka 2016 baada ya kushirikishwa na msanii Drake kwenye wimbo wake “One Dance,” ambao ulifanikiwa kupanda hadi nafasi za juu kwenye chati za Billboard katika nchi takribani 15 Duniani.
“Kati ya 2019 na 2020, Wizkid alishirikishwa katika mradi (project) ya msanii kutoka nchinj Marekani Beyonce knowles iitwayo ‘The Lion King’ kupitia wimbo maarufu uitwao “Black skin girl.”
Oktoba mwaka 2020, alitoa album yake iitwayo ‘Made in Lagos.’ albamu iliyopata mapokezi makubwa sana huku ikifanikiwa zaidi sokoni.
Made in Lagos ni album iliyojumuisha wimbo wake wa “Essence,” wimbo uliochezwa zaidi ya mara milioni 125 kwenye mtandao wa Apple Music na kutafutwa zaidi ya mara milioni 2.8 kupitia mtandao wa Shazam.
“Mwaka huu 2021, Wizkid amekuwa msanii wa Kiafrika aliyesikilizwa zaidi barani Afrika kupitia Apple Music na kuorodheshwa kwenye chati 100 bora za kila siku katika nchi takribani 60, ikiwa ni pamoja na kuchezwa kwake kila mwezi kwenye Apple Music kukua kwa zaidi ya asilimia 250 nje ya mipaka ya Afrika.
Pia ameshirikishwa kwenye Apple Music’s Today’s Hits and R&B Now playlists, , na amekuwa mgeni wa mara kwa mara kwenye vipindi vya Apple Music Radio, vikiwemo “Africa Now Radio,” “The Ebro Show,” “New Music Daily with Zane Lowe,” na “Ovo Sound Radio.”
“Asante kwa Apple Music kwa tuzo hii, ni baraka kufanya kile ninachofanya, na ninajivunia kuiwakilisha Afrika.” Alisema Wizkid kuhusu kushinda tuzo hiyo.
Licha ya ushindi wa Wizkid kwa upande wa Afrika na The Weekend kwa Duniani, Washindi wengine waliotajwa katika tuzo hizo ni Aya Nakamura, ambaye ni msanii bora wa mwaka nchini Ufaransa, na HER, aliyetajwa kama mtunzi bora wa nyimbo wa mwaka.