Serikali imesema kuelekea kilele cha maadhimishio ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania maandalizi ya mchezo wa soka wa kirafiki baina ya timu ya Tanzania na Uganda kwa wasichana na wanaume itakayochezwa siku ya kilele cha maadhimisho hayo Disemba 9, 2021 yamekamilika.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Michezo nchini, Yusufu Omary Singo leo, Disemba 7, 2021 kwenye mkutano wa Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.
Singo amesema timu zinatarajiwa kuwasili nchini lwo Disemba 7, 2021 tayari kwa mechi zote zitakazochezwa katika Uwanja wa Benjamini Mkapa ambapo mchezo utakaoanza ni kwa timu ya wanawake utakaochezwa majira ya saa 11:00 jioni na mchezo wa pili wa wanaume utachezwa saa mbili usiku.
Amesema katika mchezo huo Serikali imeweka kiingilio kidogo ili wadau wa soka waweze kuingia na kufurahia miaka 60 ya uhuru wa Tanzania yenye mapinduzi makubwa kwenye sekta mbalimbali.
Akifafanua kuhusu kiingilio kwa siku hiyo, Singo amesema kitakuwa shilingi 2000 kwa viti vya mzunguko na shilingi 5000 kwenye jukwaa la wageni maalum (VIP).
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Alfred Kidau amesema tayari timu za Tanzania zipo kambini kwa ajili ya kujinoa na mpambano huo wa kukata na shoka.
Naye, Mwakilishi wa Kampuni ya Azam ambayo ndiyo Mdhamini Mkuu wa mchezo huo, Yahya Mohamed amesema wadau wa soka ndani na nje ya nchi watarajie kuona burudani kabambe kupitia kituo cha Televisheni cha Azam.