RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameitaka Timu ya Taifa ya Tanzania ya Watu wenye Ulemavu, ‘Tembo Warriors’, ikaendeleze moto uleule Kombe la Dunia nchini Uturuki, kama iliyouonyesha kwenye michuano ya mpira wa miguu ya Afrika (CANAF), iliyomalizika mwishoni mwa juma lililopita Jijini Dar es salaam.

Akizungumza kwenye hafla aliyoiandaa ya kuwapongeza wachezaji wa Tembo Warriors, benchi la ufundi na viongozi wao, Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema kitendo cha timu hiyo kufuzu kwenda kucheza Kombe la Dunia kwa watu wenye ulemavu ni sifa kubwa kwa taifa na kuwataka kwenda pia kuipeperusha vema bendera ya Tanzania nchini Uturuki ambako fainali hizo zitafanyika Oktoba mwakani.

“Nendeni mkafanye kama ndiyo kwanza mnaanza, mafanikio haya yasiwafanye mjione sisi ndiyo sisi, mnakokwenda ni ugenini, huko nako kuna saikolojia yake, hapa mlishangiliwa vizuri kwa sababu mlikuwa na mashabiki, huko hakuna. Mimi nitakuwa pamoja nanyi, nitawapa mlezi mzuri wa kuwasimamia,” alisema Rais Samia akiwaasa na kuwakumbusha nini wanatakiwa kwenda kufanya kwenye fainali hizo.

Rais aliwapongeza wachezaji wa timu hiyo ya taifa kwani pamoja kuundwa kwa muda mchache tu mwaka 2018, lakini imepata mafanikio makubwa kwa muda mfupi, tofauti na timu zingine za michezo mbalimbali.

“Kuna timu zipo tangu nyinyi hamjazaliwa nchi hii, lakini hawajawahi kwenda michuano yoyote ya dunia. Hongereni watoto wangu, tutaendelea kuwatunza na kuwajengea mazingira mazuri ili mkienda huko nako mkafanye vizuri.

“Kombe la Dunia ni Kombe la Dunia tu, liwe la kucheza bao, kucheza karata, au mpira kwa wenye ulemavu, mradi ni fainali za Kombe la Dunia si jambo la mchezo, mmeweka historia, hakuna waliowahi kwenda huko,” alisema.

Lori laua wanafunzi wawili
Tahadhari kutoka Jeshi la Polisi