Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo leo tarehe 10 Disemba, 2021 amekabidhi Mpango Kazi wa Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira na Mwongozo wa Tuzo ya Taifa ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kwa wajumbe wa Kamati Maalumu ya Kampeni hiyo katika kikao kilichofanyika mkoani Dar es Salaam.

Katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Mohammed Khamis Abdulla, amesema Lengo la Kampeni hiyo ya miaka mitano 2021-2026 ni kuelimisha na kuhamasisha ushiriki wa jamii na uwajibikaji wa mamlaka za usimamizi katika hifadhi na usafi wa mazingira ili kuleta ustawi wa jamii ya watanzania na maendeleo endelevu.

“Nyaraka hizi ni vitendea kazi vya Kamati hii Maalumu pamoja na jamii ya watanzania katika utekelezaji wa Kampeni hii. Hivyo ninawakabidhi rasmi nyaraka hizi muhimu kama ishara ya kuwa kazi imeanza rasmi. Niwaombe mtoe uzito wa pekee katika kutekeleza majukumu hayo ya hiari ili kuwezesha kufikiwa kwa lengo la Kampeni,” Amesema Waziri Jaffo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati Maalumu ya Kampeni Kabambe Seif Ally Seif amesema kwamba, ni imani yake kuwa utekelezaji wa Kampeni hiyo utaanza mara moja na kuwa Kamati yake iko tayari kuungana na Serikali katika kuwezesha utekelezaji wake kwa ufanisi mkubwa.

Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira ilizinduliwa tarehe 5 Juni, 2021 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani na Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kampeni hii itakuwa endelevu na itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026.

Davido ajinunulia gari la kifahari kama zawadi ya Krismas.
Jaji Mkuu ateta na Mawakili