Wafanyakazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kujiepusha na mazingira yatakayowapelekea  kuomba na kupokea rushwa  kutoka kwa wagonjwa kwa kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi.

Rai hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohamed Janabi wakati wa kikao cha wafanyakazi kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Prof. Janabi amesema iwapo mfanyakazi wa Taasisi hiyo ataomba na kupokea  rushwa atajulikana hiyo ni kutokana na kuwepo kwa namba za simu za kutoa maoni na malalamiko zilizowekwa kwa ajili ya wananchi ambazo zimebandikwa katika maeneo mbalimbali ya Taasisi hiyo.

“Usifikirie kuwa utakapoomba na kupokea  rushwa hautajulikana hata kama utafanya jambo hilo kwa siri kumbuka hela za mgonjwa zinachangwa na ndugu wengi hivyo basi yule aliyekupa rushwa ili apate huduma naye pia ataenda kuwajulisha ndugu zake kuwa nimetoa hela na hivyo kulifanya jambo hilo kutokuwa la siri tena”, alisema Prof. Janabi.

“Kama una maoni au changamoto katika eneo lako la kazi mjulishe kiongozi wako ili ayafikishe katika vikao vya menejimenti na kupatiwa ufumbuzi ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma tunazozitoa kwa wananchi”, amesema Prof. Janabi.

Akitoa maoni yake katika mkutano huo e Mkuu wa Idara ya magonjwa ya Moyo kwa watoto Dkt. Sulende Kubhoja amesema mafunzo ya huduma kwa mteja yanahitajika kutolewa mara kwa mara kwa wafayakazi kwani jinsi utakavyompokea mtu  na  kumsaidia ndivyo mgonjwa atakavyoridhika kwa huduma aliyoipata.

Katika kikao hicho pia Prof. Mohamed Janabi alikabidhi fedha  taslim Tshs. 500,000/=  kwa Askari wa Kampuni ya Ulinzi ya Ng’e anayelinda  katika Taasisi hiyo Aisha Twalibu ikiwa ni zawadi ya uaminifu aliouonesha baada ya kuokota begi la ndugu wa mgonjwa lililokuwa na zaidi ya Tshs.milioni 10 na kumkabidhi muhusika baada ya kugundua kuwa amelipoteza na kulikuta kwa mlinzi huyo.

Rais Samia afanya uteuzi
Kim Kardashian azidi kumchanganya Kanye West.