Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amewataka vijana kuwa balozi namba moja wa kazi kubwa ya maendeleo inayofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi CCM chini ya mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu.
Waziri Bashungwa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Karagwe ametoa kauli hiyo Desemba 13, 2021, wakati akizungumza na vijana kutoka sehemu mbalimbali za Wilaya ya Karagwe katika baraza la umoja wa vijana wa chama hicho lililofanyika ukumbi wa CCM Karagwe.
“Vijana hakikisheni mlipo mama Samia awepo, tuna sababu ya kutembea kifua mbele kama vijana tukiinadi kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita inayo ongozwa na Mama Samia kwa sababu wote tunaona kwa macho namna kazi inavyo endelea kisawasawa” Alisema Waziri Bashungwa.
Akizungumza kwa niaba ya vijana Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya Karagwe Alexius Sylivester amempongeza Waziri Bashungwa kwa namna anavyopambana kutekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa na CCM katika jimbo hilo.
“Mhe. Mbunge sisi UVCCM kabla ya baraza hili, tulifanya ziara katika kata zote 23 za jimbo la Karagwe kuangalia Uhai wa chama na jumuiya zake pamoja na utekelezaji wa Iilani ya Chama Cha Mapinduzi, naomba nikupongeze adharani kwa kazi kubwa unayoifanya, kwa sababu tumegundua kuwa Chama kiko imara na kazi inaendelea” Alisema Alexius
Kwa Mujibu wa Alexius kikao hicho cha Baraza la UVCCM Karagwe ni kikao cha kikanuni kwa ajili ya kufanya tathimini za kazi za Jumuiya ya vijana wa Chama Cha Mapindzi ndani ya wilaya hiyo.