Kikosi cha Azam FC leo Jumanne (Desemba 14) kimefanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuanza Mshike Mshike wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kesho Jumatano (Desemba 15).
Azam FC wataanza Michuano hiyo kwa kuikaribisha Green Warrios, katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam kuanzia saa kumi jioni.
Taarifa ya kuthibitisha maoezi ya mwisho kwa wachezaji wa Azam FC imechapishwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya klabu hiyo.
“Vijana wamemaliza salama mazoezi ya mwisho leo Jumanne asubuhi kujiandaa na mchezo wa raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) dhidi ya Green Warriors utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho saa 10.00 jioni.”
Kikosi cha Azam FC kitashuka Dimbani kwa mara ya kwanza msimu huu bila ya Kocha Mkuu Goerge Lwandamina aliyesitishiwa mkataba wake klabuni Jana Jumatatu (Desemba 13), kufuatia mambo kumuendea kombo kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mbali na Lwandamina, Kocha Msaidizi Vivier Bahati naye hatokuwa sehemu ya Benchi la Ufundi, kutokana na maamuzi ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo.
Kikosi cha Azam FC kwa sasa kinanolewa kwa muda na kutoka Marekani mwenye asili ya Somalia Abdihamid Moallin.
Moallin ameajiriwa klabuni hapo kama Mkurugenzi wa Ufundi wa kituo cha kukuza vipaji (Azam FC Academy).