Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, amesema kikosi chake kitapaswa kucheza kwa heshima dhidi ya Ihefu FC, katika mchezo wa Mzunguuko wa tatu wa Kombe la Shirikisho leo Jumatano (Desemba 15) Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam.
Nabi amesema katika mashindano hakuna timu ndogo, kila mchezo kwao ni muhimu kupata matokeo mazuri hasa ukizingatia michuano hii ni ya mtoano na mshindi hupata nafasi ya kuwakilisha nchini, Kombe la Shirikisho Afrika.
Amesema kikosi chake kipo imara na wanaenda kupambana kutafuta matokeo mazuri katika mchezo huo ambao ni muhimu kwao kushinda.
“Hakuna mchezo rahisi, kila mmoja anahitajj matokeo mazuri tumefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mchezo uliopita ikiwamo kutengeneza nafasi na kuzitumia vema ili kupata ushindi,” amesema Nabi.
Msimu uliopita Young Africans ilifika Fainali ya ASFC na kufungwa bao 1-0 na Mabingwa watetezi Simba SC mjini Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika, bao likifungwa na kiungo kutoka nchini Uganda Thadeo Lwanga.