Kocha wa Mkuu wa Ihefu FC, Zuberi Katwila amesema kikosi chake kipo tayari kuikabili Young Africans kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ mzunguuko wa tatu.

Ihefu FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu huu, itakuwa mgeni wa Young Africans saa moja jioni leo Jumatano (Desemba 15), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha Katwila amesema kikosi chake kimefanya maandalizi mazuri na wanaiheshimu Young Africans ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri, lakini hawataogopa majina ya nyota hao, na wataingia uwanjani kupambana mwanzo mwisho.

“Mechi itakuwa na ushindani mkubwa kwa sababu kila mmoja anahitaji matokeo ili kusonga mbele, ukizingatia wapinzani wetu wameimarika vizuri, lakini tumejiandaa vizuri kwenda kuleta ushindani,” amesema Katwila.

Mchezo huo utakumbushia mchezo wa mwaka 2018, ambao Young Africans ilipata upinzani mkali kutoka kwa timu hiyo yenye maskani yake Mbarali, Mbeya, wakati huo kabla haijapanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2020/21, na kisha kushuka tena msimu huo huo.

Mchezo huo mkali uliopigwa Januari 30, 2018 kwenye uwanja wa Sokoine, Young Africans ilipata wakati mgumu ikionekana imeshalala, ikisawazisha bao dakika za majeruhi na kushinda kwa mikwaju ya Penati 4-3.

Wakati huo huo Azam FC nayo itakuwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi kucheza dhidi ya maafande wa Green Warrios kwenye mchezo wa Mzunguuko wa tatu wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ utakaochezwa saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Azam itacheza mchezo huo bila George Lwandamina, aliyejiuzulu nafasi yake juzi Jumatatu (Desemba 13) kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwa maslahi ya klabu.

Kikosi cha Azam FC kitakuwa chini ya Abdihamid Moalim kwa mara ya kwanza, akikaimu nafasi ya Kocha Mkuu. Moalim hivi karibuni alitangazwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo.

Rais Samia ajibu ombi la Zitto Kabwe
Wachezaji Young Africans watahadharishwa